Bodi ya Tumbaku Tanzania ni chombo cha udhibiti wa zao la tumbaku kilichoanzishwa chini ya sheria ya sekta ya tumbaku Na. 24 ya 2001 (kama ilivyorekebishwa na sheria ya mazao (marekebisho mchanganyiko) Na. 20 ya 2009). Majukumu makuu ya udhibiti ya Bodi kama yalivyoelezwa katika sehemu ya tano (5) ya sheria ya tumbaku ni:-

  1. Uundaji, utekelezaji na usimamizi wa miongozo na viwango vya sera vinavyolenga kudhibiti na kuboresha utendaji wa tasnia ya tumbaku nchini Tanzania;
  2. Kutoa ushauri kwa Waziri anayehusika na Kilimo na Serikali kwa ujumla juu ya masuala yote yanayohusiana na Sekta ya tumbaku; na
  3. Uhamasishaji na uendelezaji wa mazingira mazuri kwa ajili ya ufanisi na ushindani kwa wadau wote katika sekta ya tumbaku.

DIRA

Kuwa bora katika utoaji wa huduma za udhibiti, ushauri na ukuzaji wa sekta ya tumbaku.

DHAMIRA

Kutoa huduma kwa wakati na ubora kwa wakulima na wafanyabiashara wa tumbaku katika suala la usajili, ushauri wa kitaalam na uwezeshaji wa mchango wa sekta binafsi katika sekta ya tumbaku kwa ukuaji bora na endelevu kwa manufaa ya sekta na nchi.

Shughuli Kuu

Shughuli kuu za Bodi ni kukuza, kuendeleza na kudhibiti tasnia ya tumbaku nchini Tanzania.

Historia ya Bodi ya Tumbaku

Historia ya Bodi ya Tumbaku inarudi miaka ya 1960 wakati Serikali ilipoanzisha Bodi ya Tumbaku ya Tanganyika. Mnamo mwaka 1970 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianzisha Mamlaka ya Tumbaku ya Tanzania (TAT). TAT ilibadilishwa mnamo 1984 kuwa Bodi ya Usindikaji wa Tumbaku na Masoko Tanzania (TTP & MB).

Mnamo mwaka 1993 TTP & MB ilirekebishwa tena kuwa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kufuatia ubinafsishaji wa sekta ya tumbaku ambayo ilifikia kilele mnamo 1997 wakati shughuli za Bodi ya Tumbaku zilipofadhiliwa na Serikali. Bodi ya sasa ni matokeo ya Sheria ya Sekta ya Tumbaku Na.24 ya 2001, na marekebisho yake ya mwaka 2009.