Uzalishaji wa tumbaku hufanyika kupitia kilimo cha mkataba. Kilimo cha mkataba kimefanywa katika sekta ya tumbaku kwa miaka mingi. Tumbaku nchini huzalishwa zaidi kwa utaratibu wa kimkataba kupitia kilimo cha mkataba kwa kushirikisha pande mbili yaani mnunuzi wa tumbaku na wakulima. Awali hii ilihusisha mnunuzi kusambaza pembejeo za kilimo ikifuatiwa na masoko ya tumbaku. Mnunuzi ananunua tumbaku kutoka kwa mkulima. Kama ilivyo sasa, mkataba unategemea hasa makubaliano kwa mnunuzi kununua tumbaku inayozalishwa (Mikataba ya ununuzi wa tumbaku mbichi).

Mageuzi ya sasa ya zao la tumbaku yameleta mabadiliko muhimu kwenye kilimo cha mkataba kama ilivyo desturi katika sekta ya tumbaku. Mipango ya kilimo cha mkataba ya awali iliwashirikisha wanunuzi na wakulima tu. Wadau wengine hawakuhusika. Kama sehemu ya mageuzi katika zao, kumekuwa na marekebisho katika sheria ya sekta ya tumbaku ili kupanua wigo na taratibu za kilimo cha mkataba katika sekta ya tumbaku ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi za kifedha, wauzaji wa pembejeo, wawekezaji, wasindikaji na mtu yeyote mwenye nia ya kusaidia mkulima wa tumbaku kwa kuzingatia makubaliano.

Chini ya mageuzi ya sasa, mageuzi ya kilimo cha mkataba yanatambua jukumu la wadau wote wa tumbaku katika kuwezesha uzalishaji wa tumbaku. Pia huunda sauti na kulinda uhusiano wa kibiashara kati ya mkulima wa tumbaku na wadau wengine hasa wanunuzi wa tumbaku, mabenki, wasambazaji wa pembejeo na wawekezaji wengine wanaohusika katika kukuza ukuaji endelevu wa zao la tumbaku nchini.

Kilimo cha mkataba cha sasa kama amabvyo kimekuwa kikifanyika katika sekta ya tumbaku kitasaidia kulinda maslahi ya wakulima wa tumbaku na wawekezaji kama utaratibu muhimu wa wadau wa tumbaku. Kimsingi kitalinda maslahi ya wadau wa tumbaku kwa ujumla katika kuendeleza malengo ya ASDP na kujenga mazingira ya biashara na uwekezaji kwa ajili ya ukuaji endelevu wa zao la tumbaku nchini.

Zaidi ya yote, chini ya kilimo cha mkataba kilichofanyiwa marekebisho, kanuni ya uhuru wa mkataba imezingatiwa sana kwani mpaka sasa kilimo cha kimkataba huhusisha mazungumzo kati ya pande huru na kipindi cha kimkataba kuwa kwa msimu wa kilimo katika mwaka husika, nakutoa fursa ya kurefusha kipindi cha mkataba kwa kupitiwa upya na pande zote mbili. Kuna pia jitihada zinazoendelea upande wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kujumuisha sehemu maalum ya kilimo cha mkataba katika mswada ujao wa usimamizi rasilimali za kilimo.